JOSE MOURINHO AMPIGA MKWARA RASHFORD
JOSE MOURINHO AMPIGA MKWARA RASHFORD
MWACHENI Jose Mourinho na kiburi chake aisee. Ungeweza kudhani angetoa maneno ya kufariji kwa kinda Marcus Rashford baada ya juzi kuibuka na ushujaa wa dakika za mwisho katika pambano gumu dhidi ya Hull City ugenini. Mourinho bado hajalainika kirahisi hivyo.
Rashford alitokea katika benchi akichukua nafasi ya Juan Mata katika dakika za mwisho za pambano hilo la kusisimua lililopigwa Uwanja wa KCOM jijini Hull na dakika chache baadaye akaifungia Man United bao la ushindi.
Rashford bado hajaanza mechi yoyote chini ya Mourinho licha ya kutamba katika msimu uliopita akiwa na Kocha aliyetimuliwa, Louis van Gaal kiasi cha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kilichoshiriki michuano ya Euro nchini Ufaransa.
Kwa sasa ametoswa na kocha mpya wa England, Sam Allardayce kwa sababu hiyo hiyo ya kutochezeshwa na Mourinho huku akimpeleka katika kikosi cha timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 21.
Hata hivyo, licha ya kufunga bao muhimu jana, Mourinho amedai kwamba bao hilo halijamshawishi kuanza kumpanga Rashford tangu mwanzo kwa sababu inabidi afanye kazi kwani, wachezaji wanaoanza wamekuwa wakifanya kazi nzuri.
“Sio kwa sababu amekuwa mshindi wa mechi basi nitabadili mawazo. Huwezi kutompanga mchezaji mwingine wakati wanaoanza wanacheza vizuri. Mshambuliaji wetu namba moja (Zlatan Ibrahimovic) ni mchezaji hatari. Si tu kwamba ni mfungaji lakini anacheza vyema kitimu.
Anatengeneza nafasi,” alisema Mourinho.
“Ni kweli tunaweza kuanza na mchezaji mwingine mbele ya Zlatan lakini inabidi utawale sana uwanjani ili ulingane naye. Rashford anaweza kucheza au kukaa katika benchi. Hata hivyo, atacheza mechi nyingi msimu huu. Najua alikuwa mzuri msimu uliopita na sasa nafanya naye kazi kila siku na nafikiria hivyo. Alitupa mbinu tofauti alivyoingia.”
Mourinho alikiri kwamba timu yake ilikuwa imeshinda katika dakika za Sir Alex Ferguson, lakini aliamini kuwa bao lilikuwa njiani linakuja huku pia akiipigia saluti safu ya ulinzi ya Hull City ambayo ilicheza kwa ushirikiano mkubwa ndani ya dakika 90 mpaka Rashford alipofunga bao la ushindi kwa krosi fupi ya Wayne Rooney.
“Sir Alex Ferguson ni mtu anayeheshimika katika klabu hii na nina furaha kusema kwamba tulishinda katika muda wa Fergie. Nina furaha sana kusema hivyo,” alisema Mourinho ambaye anajulikana kwa tabia yake ya kumheshimu kocha huyo mkongwe wa Scotland.
“Najua tunapofunga mwishoni watu watasema kuna bahati kidogo lakini ukweli ni kwamba tulistahili, sana sana katika kipindi cha pili. Tulitawala sana mechi, tulicheza kwa nguvu kasi tukishambulia na niliamini kuwa bao lingekuja tu,” alisema Mourinho.
“Inabidi niseme kwamba Hull City walifanya kazi ya ajabu na walijilinda sana kwa kila namna. Hawakuweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa sababu naamini tulijilinda vizuri sana. Hongera kwao na kama ningekuwa Mwenyekiti wao ningempa kazi ya kudumu kocha Mike Phelan haraka sana.”
“Kila mtu anaona kwa macho yake, wachezaji wanatoa kila walichonacho kwa ajili yake. Wasingeweza kufanya zaidi ya kile walichofanya na hongera sana kwa Mike na vijana wake,” alisema Mourinho ambaye kwa ushindi huo United yake inakuwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za mwanzo dhidi ya Southampton, Bournemouth na Hull City juzi usiku.
Hata hivyo, mtihani wa kwanza halisi kwa United unatazamiwa kuwa dhidi ya Manchester City katika pambano lijalo la Ligi Kuu baada ya mechi za kimataifa zinazotazamiwa kuchezwa wikiendi ijayo.
Pambano hilo litachezwa Septemba 10 huku likitazamiwa kuwakutanisha makocha wawili mahasimu wa muda mrefu, Jose Mourinho na Pep Guardiola wa Manchester City.
No comments