HITAJI LA MOYO SEHEMU YAA KWANZA
MWANDISHI/MTUNZI :Gaooh Mussah
Whatsapp 0654387935
Kisa cha kwanza Usaliti 1
Hitaji la mwanadamu ni kuishi kwa furaha, furaha iliyomezwa na
amani ya moyo. Furaha ya maisha itakayoziba machungu na maumivu hasa kwa kila mwanadamu.
Naamini kila mmoja hupenda furaha si furaha ya usoni laa hasha! bali furaha ya
moyo itakayomwacha na tabasamu pana kila wakati na kumsahaulisha maumivu ya
maisha na mapenzi.
Mbali na maumivu yale ya penzi lakini hayakumbadilisha, jambo
hisia liliteka nafasi kubwa ya moyo wake pasi na kumpa nafasi ya kuruhusu
mawazo kumbadilisha.
Hakika moyo wa kupenda hauna mtetezi. Hupendelea kusimama pale
unapopenda. Moyo umejaa uvumilivu usio na kigeugeu cha kubadili maamuzi kwa
muda mfupi. Moyo ni rafiki mwema kwa mwanadamu tofauti na nafsi iliyoumbwa kwa
tamaa za kutamani visivyo vyake kiasi cha kujiumbia maumivu ambayo huenda
yanaweza epukika.
Nafsi inashindwa kuiga
mfano wa moyo na kufanya vile itakavyo. Mwisho wa siku nafsi inaishia kujisuta
yenyewe na kukosa wapambe wa kuipaka majivu.
Ukubwa wa jina la shule na
sifa zake kutokana na kuanzishwa kwake muda mrefu kiasi cha kubeba
historia ya wilaya, ndiyo ilikuwa
kitambulisho pekee cha kuitambulisha shule ile ya kata, mbali na ufaulishaji
wake kwa wanafunzi hasa baada ya mitihani wanafunzi wengi kupata alama nzuri za
kujiendeleza na elimu za juu.
Naam! Iliitwa Mazinde Day Secondary School, jina ambalo
lilipatikana kutokana na jina la kata hiyo kwa vile ni shule ya kwanza
kuanzishwa katika kata hiyo ambayo iliitwa Mazinde inayopatikana katika
mgawanyo wa wilaya mbili za Korogwe nikimaanisha Korogwe mjini na Korogwe
vijijini. Kata hiyo ya Mazinde ilifunikwa na mwamvuli wa Korogwe vijijini huku
tarafa yake ikiwa ni Mombo.
Shule hiyo ilipata kuanzishwa mwaka 1995 baada ya kuwa hospitali
ya wajerumani ndipo ilibadilishwa na kuwa shule. Shule ya sekondari ikiwa
katikati ya mashamba ya mkonge.
Sifa za shule hiyo kutokana na ufaulishaji wake
na sifa nyingine mbali mbali, ndiyo ilikuwa silaha kubwa ya kujizolea wanafunzi
wengi, tena wengine wakitoka mbali na mkoa wa Tanga.
Binti aliyetambulika kwa jina la Natasha
alikuwa miongoni mwao hasa akitokea mkoa mwengine tofauti na Tanga,
Alitokea mkoa wa Morogoro jiji kasoro bahari,
alikozaliwa msanii mkubwa wa Bongo fleva Belle 9 hutakosea ukimwita Belle tisa
au jina lake halisi Abelnego.
Natasha alipendeza kwa muonekano wake, hasa akibeba umbo lisilo na
ubaguzi wa nguo. Kila nguo ilimkaa na kumpendeza.
Haikuishia hapo alipewa rangi halisi ya mtanzania nikimaanisha
nyeusi, huku mdomoni meno yake yakiacha mwanya mdogo ulioyapendezesha. Alipewa
zawadi ya macho yaliyojaa hamasa ya kuangaliwa kila mara, kiasi cha kufanya
wamtazamao wasichoke kutazamana naye.
Haikuishia hapo,umbo namba nane kama sio saba lilimpendeza vyema.
Guu la bia na hipsi za haja hazikuacha kuonesha uwepo wake kwenye mwili wa
Natasha.
Natasha alijiunga na shule hiyo akianzia kidato cha kwanza. Alikaa
katika mabweni ambayo hayakuwa rasmi, kwavile shule hiyo serikalini
ilitambulika kuwa ni shule ya kutwa hivyo hata mabweni yake hayakuwa mengi
zaidi ya majengo mawili tu tena yakiwa ya jinsia ya kike pekee. Wavulana
hawakuwa na nafasi ya kuishi ndani yake.
Uzuri wa Natasha sambamba na heshima na adabu pamoja na upole
vilikuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi
wenzake kiasi cha kumpenda. Hakuwa mbaguzi. Aliwajali wanawake kwa wanaume.
Alikuwa na tabia njema ambazo zilikuwa ni mfano wa kuigwa na wengine.
Mbali na uzuri aliokuwa nao mpaka kufikia wakati huo akiwa kidato
cha kwanza hakuwa akimjua mwanaume yeyote. Hapa ninamaanisha alikuwa hajaijua
safari ile ya mapenzi, japo aliwahi kusumbuliwa na wanaume kadhaa huko Morogoro
akiwa masomoni lakini hakuwakubali.
Kutokuwa na mpenzi ndio lilikuwa jambo bora lililomkusanyia
marafiki wa kutosha. idadi ya marafiki zake ilimezwa na wingi wa marafiki wa
kiume japo alikuwa na marafiki hao lakini haikumfanya aingie katika vishawishi
nao.
Alikijali kilichompeleka shuleni ambacho ni masomo pekee. Hakuwa
na muda wa kusikiliza maneno yoyote yasiomfaa. Hiyo ikawa silaha kubwa ya kuwakata
vilimi wale waliokuwa na tamaa naye.
Japo uzuri wake ulimfanya apitie vishawishi vingi kwa wanaume,
lakini haikumbadilisha msimamo wake alioushikilia. Vile vile hakutaka kuwa na
mpenzi kwa wakati huo .
Maisha ya shule nayo yaliendelea huku siku nazo zikiteketea. Siku
hizi zilifanikiwa kumbadili badala ya kuwa mgeni sasa alikuwa mwenyeji wa shule
hiyo.
Alipendwa na kila rika hata walimu walivutiwa naye kwa tabia yake
ya kuwajali wengine. Looh! Hakujua kijacho mbele yake.
Natasha John alivutika na ushawishi wa kijana aliyeitwa Hudson
Aidan. Kijana huyu alimzidi kidato kimoja. Natasha akiwa kidato cha pili na
Hudson akiwa kidato cha tatu.
Looh! Hakujua ya ndani ya
kijana yule. Furaha pekee ilikuwa kupendwa naye akiamini amepata wa
kumpenda tena akijiona kachelewa kupendwa nae. Hakika usilolijua sawa na usiku
uliojaa giza.
Hudson alimwumiza Natasha kwa kumsaliti. Kisingizio ni kukosa
penzi kwake.
Hilo lilimuuma sana Natasha. Msimamo aliyojiwekea wa
kutojishughulisha na mapenzi mpaka aingie kwenye ndoa ndio yalikuwa malipo
yake.
Ndugu msomaji penzi ni msumali ugongao mahali pasipostahili
kugongwa. Natasha alitupa jiwe sokoni.
ITAENDELEAA.
Burudika nasi, na ujifunze nasi
No comments